Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) kupitia kwa Mtendaji wake Mkuu Boniface Wambura imetangaza msimu mpya wa ligi hiyo 2018/19 kuanza kutimua vumbi rasmi tarehe 22/08/2018 ukishirikisha timu 20. Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na bodi hiyo, watani wa jadi Simba na Yanga wamepangwa kukutana Septemba 30 mwaka huu ambapo Simba watakuwa wenyeji. Wambura amesema ratiba hiyo imezingatia ratiba ya michuano mingine ikiwemo michuano ya CAF itakayoanza mwezi Novemba mwaka huu, kalenda ya FIFA, Kombe la Mapinduzi pamoja na michuano ya CECAFA. Mechi ya ngao ya jamii kuashiria kuanza kwa msimu mpya wa ligi itapigwa Agosti 18, 2018 kwenye dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza, na itakuwa ni kati ya mabingwa wa ligi kuu msimu uliopita Simba SC dhidi ya Mtibwa Sugar ambao ni mabingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports. Tarehe 22/08/2018: Simba SC vs Tanzania Prisons, Ruvu Shooting vs Ndanda FC, Alliance vs Mbao FC, Coastal Union vs Lipuli FC, Singida United vs Biashara, Kagera Sugar vs Mwadui FC. Tarehe 23/08/2018: Stand United vs African Lyon, JKT Tanzania vs KMC, Mtibwa Sugar vs Yanga SC, Azam FC vs Mbeya City.
Straika wa Lipuli FC ya Iringa Adam Salamba ambaye alijiunga na timu hiyo akitokea Stand United ya Shinyanga, ghafla amerejea Shinyanga yalikokuwa makazi yake na anakutana na Dodi katika kipindi cha Soka Kijiweni. Amezungumza mengi akiwa na washkaji zake likiwemo lile bao aliloifunga Simba katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Lipuli. Katika hali ya kushangaza pia mtangazaji Baraka mpenja kutoka Azam TV ameibuka na kuwapa LIVE lile bao la pili alilofunga Habib Kiyombo wa Mbao FC dhidi ya Yanga, Desemba 31, 2017. Hii ni sehemu ya kipindi kilichoruka Aprili 30 mwaka huu. Kumbuka kipindi hiki kila Jumatatu saa 1:00 usiku, Azam Sports 2.
Mwadui FC imepanda kutoka nafasi ya 12 hadi ya 9 kwenye msimamo baada ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Mbao FC kwenye mechi ya Ligi Kuu soka Tanzania Bara iliyochezwa leo jioni Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga. Bao pekee la Mwadui FC limefungwa dakika ya 29 na Charles Ilanfya aliyetumia vyema makosa ya golikipa Mussa Mohamed wa Mbao FC ambaye alipiga kimakosa mpira aliombabatiza mchezaji wa Mwadui FC, Salim Khamis. Hata hivyo, Mwadui walilazimika kucheza pungufu kwa dakika 38 za kipindi cha pili kutokana na golikipa wake, Anord Massawe kuoneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kufuatia kuudaka mpira nje ya eneo lake akiwa mchezaji wa mwisho.
Mwadui FC wameibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbao FC, bao pekee likifungwa na Charles Ilanfya kutoka na makosa ya mawasiliano yaliyofanyika kati ya golikipa na mabeki wao. Ni mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) uliopigwa leo kwenye dimba la Mwadui Complex, Shinyanga.
Tazama jinsi timu ya Mbao FC ilivyobanwa mbavu na Lipuli FC katika dimba lake la CCM Kirumba Mwanza na kulazimishwa suluhu katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara (VPL) uliopigwa Ijumaa Aprili 6, 2018. Katika mchezo huo Mbao walitengeneza nafasi nyingi ndani ya eneo la 18 la Lipuli lakini walishindwa kufunga, huku pakitokea kituko cha gloves za kipa wa Lipuli kuibiwa na kutupwa nje ya uwanja tukio ambalo lilitokea dakika ya 45.
Mbao FC imeshindwa kutumia vyema uwanja wake wa nyumbani (CCM Kirumba) baada ya April 6 kulazimishana suluhu na Lipuli katika mchezo wa Ligi Kuu. Katika mechi hiyo wakati wa mapumziko, palizuka vurugu kwa makomandoo wa timu zote mbili na kusaidiwa na Askari Polisi waliofika kutuliza ghasia hizo.