Bao pekee kutoka kwa beki Abdallah Haji Shaibu ‘Ninja’ limetosha kuipa Yanga pointi tatu mbele ya African Lyon katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha. Ninja amefunga goli hilo kwa kichwa dakika ya 64 akimalizia mpira wa adhabu ndogo ulipigwa na Ibrahim Ajibu, bao lililodumu hadi mwisho wa mchezo na kuendeleza rekodi ya ushindi na kutopoteza mchezo kwa Yanga tangu kuanza kwa ligi msimu huu. Ushindi huo unaifanya Yanga izidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha pointi 47, mbele ya Azam wenye pointi 40 na Simba wenye pointi 30.