Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wamepata ushindi wa mabao 2-0 wakiwa ugenini dhidi ya JKT Tanzania, mchezo ukipigwa kwenye Dimba la Mkwakwani mkoani Tanga. Mabao yote ya Simba yamefungwa na mshambuliaji wao Meddie Kegere dakika ya 12 na 38, kazi nzuri ikifanywa na Emmanuel Okwi. Mshambuliaji wa JKT Tanzania Ally Ahmed Shiboli ambaye aliingia kutokea benchi, alikumbana na rungu la mwamuzi Mbaraka Rashid baada ya kuonesha kitendo cha utovu wa nidhamu dhidi ya mwamuzi huyo. Tukio hilo limetokea dakika ya 88 wakati wachezaji wa JKT Tanzania wakidai kunyimwa penati baada ya mpira kumgonga mkononi beki wa Simba, Erasto Nyoni. Mchezo huu pia ulikumbwa na tafran dakika za mwisho. Baada ya mchezo, upande wa JKT ulikataa kufanya mahojiano, huku upande wa Simba akizungumza nahodha wao John Bocco.