Simba SC imebakiza pointi mbili katika michezo mitatu iliyosalia kutetea taji lake la Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya leo kuichapa Ndanda SC kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam na kufikisha pointi 88 kileleni mwa msimamo wa ligi. Mabingwa hao watetezi wamepata ushindi wa mabao 2-0 yote yakifungwa na Meddie Kagere ndani ya dakika kumi, akianza dakika ya 6 kwa pasi ya John Bocco, kisha dakika ya 11 kwa pasi ya Clatous Chama. Mabao hayo yamemfanya Kagere kufikisha jumla ya magoli 22 kwenye ligi kuu msimu huu, akimuacha kwa mbali mshambuliaji wa Yanga Heritier Makambo na mshambuliaji wa Mwadui FC Salim Aiyee wenye magoli 16 kila mmoja, huku Emmanuel Okwi na John Bocco wa Simba pia wakiwa nyuma yao na mabao 15 kila mmoja. Baada ya mchezo wa leo, Simba inasafiri kwenda mjini Singida ambako itacheza na Singida United Jumanne ya Mei 21, 2019, na endapo watapata ushindi basi shughuli itakuwa imekwisha msimu huu kwani watakuwa wamefikisha pointi 91 ambazo hazitaweza kufikiwa na timu yoyote. Kwa upande wao Ndanda SC wameendelea kubaki kwenye nafasi yao ya nane wakiwa na pointi 47 na wamekiza mechi mbili ambzo zote watacheza nyumbani kwao Mtwara.