Mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga SC leo imepata ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Stand United katika mchezo wake wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa leo kwenye Dimba la Taifa Dar es Salaam. Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua, Yanga imeanza mapema kutikisa nyavu za Stand baada ya Mrisho Ngasa kuitanguliza kwa bao la dakika ya 2, kabla ya Stand kusawazisha kupitia kwa Alex Kitenge dakika ya 15. Mchezo ulizidi kuwa mkali ambapo Yanga walipata mabao mawili ya haraka haraka kupitia kwa Ibrahim Ajib dakika ya 32 na Andrew Vincent dakika ya 35 matokeo yaliyodumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Yanga kutangulia kufunga bao la nne kupitia kwa Deus dakika ya 57 akiitumia vyema pasi aliyopewa kwa kichwa kutoka Ibrahim Ajib, lakini Stand United walijibu na kufunga bao la pili dakika ya 59 kupitia kwa Alex kitenge tena. Wakati wengi wakidhani kuwa matokeo ni 4-2, Alex Kitenge aliifungia Stand bao la tatu na kufanikiwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga hat-trick msimu huu, matokeo yakiwa 4-3. Matokeo hayo yanaifanya Yanga ifikishe pointi 6 baada ya kushinda mechi zake zote mbili ikiwa nafasi ya saba huku Stand wakiwa nafasi ya tisa na pointi 6.