Kwa mujibu wa kipindi hiki cha terehe 08/11/2018, bao la pili alilofunga Meddie Kagere kwenye mchezo kati ya JKT Tanzania vs Simba SC uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga Jumamosi ya Novemba 2, 2018, halikuwa bao halali kwa kuwa mfungaji alikuwa ameotea kabla ya kufunga. Pamoja na matukio mengine yaliyojiri kwenye mchezo huo, pia palikuwa na matukio mawili ya wachezaji wa JKT kudai penati wakidai wachezaji wa Simba Mohamed Hussein na Erasto Nyoni kwa nyakati tofauti, walishika mpira ndani ya eneo la hatari hadi kusababisha mchezaji wa JKT Ahmed Shiboli kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Mbali na mchezo huo, kipindi hiki kimechambua mechi kdhaa za raundi ya 13 ya Ligi Kuu Tanzania Bara ukiwemo mchezo wa Yanga vs Ndanda SC na ule wa Kagera Sugar vs Azam FC. Tukio kubwa katika mchezo wa Kagera Sugar na Azam FC ni mchezaji wa Azam FC Donald Ngoma kupewa kadi nyekundu, kadi ambayo wengi hawakuelewa sababu za adhabu hiyo kumkumba. Waamuzi wawili wastaafu ambao ni magwiji, Osman Kazi na Omary Abdulkadir wamechambua matukio yote na kuonesha ni wapi waamuzi walikosea na wapi waamuzi walipatia, na nini walipaswa kufanya. Kipyenga cha Mwisho ni kila Alhamis saa 3:30 usiku Azam Sports 2.