Timu ya Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro, imetupwa nje ya michuano wa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya leo kuchapwa 2-1 na KCCA ya Uganda katika mchezo wa maruadiano uliopigwa kwenye Dimba la Chamazi Dar es Salaam. Kwenye mchezo huo, KCCA ndiyo waliotangulia kupata bao dakika ya 28 kupitia kwa Muzamiru Mutyaba kabla ya Salum Kihimbwa kusawazisha dakika ya 51, na kisha wageni hao kutoka Jijini Kampala Uganda kupata bao la pili dakika ya 87 kupitia kwa Allan Okello. Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Jijini Kampala nchini Uganda, KCCA ilipata ushindi wa mabao 3-0, na hivyo inafuzu kuingia hatua ya mtoano kwa jumla ya magoli 5-1, huku Mtibwa ambayo hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kushiriki michuano ya CAF tangu mwaka 2002, ikifungashiwa virago.