Mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC wameendeleza ubabe wao kwenye ligi hiyo msimu huu baada ya leo kuiadhibu Mwadui Fc kwa kipigo cha mabao 3-1, mchezo ukipigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Dimba la Taifa Dar es Salaam. Mabao ya Yanga yamefungwa na Ibrahim Ajibu kwa ‘free-kick’ dakika ya 12, Amissi Tambwe dakika ya 39 akimalizia pasi ya Ibrahim Ajibu na Feisal Salum kwa shuti kali nje ya 18 dakika ya 58 huku bao la kufutia machozi la Mwadui likifungwa na Salim Aiyee dakika ya 82. Mbali na kupatikana kwa mabao hayo, Ibrahim Ajibu alikosa mkwaju wa penati iliyopanguliwa na golikipa wa Mwadui FC Anold Masawe dakika ya 19. Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 53 na kuzidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi huku wanaowafuatia Azam Fc wakiwa na pointi 40 na mchezo mmoja mkononi.