Golikipa Nouridine Balora anayeichezea Biashara United amekumbana na sakata lingine la kufungiwa mechi tano ikidaiwa kuwa alionesha utovu wa nidhamu kwa uongozi wake. Kocha wa timu hiyo Amri Said amethibitisha taarifa hizo mara baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya Biashara United na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Karume Musoma, huku akieleza kushangazwa na vitendo vinavyofanywa na golikipa huyo raia wa Burkina Faso. Kwenye mchezo huo Biashara United imeifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1. Hivi karibuni, kipa huyo alikwaruzana hadharani na kocha wake Amri Said wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports dhidi ya Yanga uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam baada ya kocha huyo kumtoa nje.