Kikosi cha Azam FC kimeshuka dimbani Azam Complex Chamazi kujipima nguvu na Timu ya Taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 23 ambapo Azam FC imepata ushindi wa mabao 2-0. Bao la kwanza la Azam FC limefungwa na Enock Atta dakika ya 12 ya mchezo huo wa kirafiki huku dakika ya 87 Obrey Chirwa akifunga bao la pili ambalo ni la kwanza kwake tangu alipojiunga na timu hiyo hivi karibuni. Wakati Azam FC ikijiandaa na mechi zake zinazofuata za Ligi Kuu Bara, timu hiyo ya Taifa chini ya miaka 23, wao wanajianda na mchezo wa marudiano dhidi ya Burundi ambao ni wa kufuzu Kombe la Afrika mwakani. Katika mchezo wa awali, Burundi ilishinda mabao 2-0 nyumbani na mchezo wa marudiano utachezwa Jumanne ijayo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.