Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC wameng’ang’aniwa kwenye Uwanja wa Uhuru kwa kulazimishwa sare ya bila kufungana na Azam FC. Timu zote zilionesha soka la kiwango cha juu ambapo Simba walifanya mashambulizi mengi zaidi langoni kwa Azam lakini walishindwa kupata bao kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Azam iliyokuwa chini ya Agrey Moris na Yakubu Mohamed. Licha ya kushambuliwa zaidi, Azam walipoteza nafasi mbili za wazi kupitia kwa Donald Ngoma dakika ya 29 na Obrey Chirwa dakika ya 87, hivyo mchezo kumalizika kwa suluhu. Matokeo hayo yanaifanya Simba kubakiza pointi nane pekee ili kutetea taji lake, ikiwa imefikisha pointi 82 na mechi tano mkononi, wakati wapinzani wao wa karibu, Yanga wakiwa na pointi 81 na mechi tatu mkononi. Azam wao wanaendelea kukaa nafasi ya tatu wakifikisha pointi 69 na mechi mbili mkononi.