Bao pekee la Hassan Dilunga likifungwa dakika za majeruh, limetosha kuipa Simba pointi tatu muhimu dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliopigwa leo kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam. Dilunga amefunga goli hilo akimalizia pasi ya Emmanuel Okwi wakati zikiwa zimebaki sekunde chache mpira kumalizika katika mechi ngumu na ya ushindani wa aina yake. JKT walionekana wagumu zaidi hasa katika safu yao ya ulinzi iliyoweza kudhibiti mashambulizi makali ya Simba hadi ilipofika dakika ya 90 kabla ya dakika saba kuongezwa lakini Dilunga akafanikiwa kufunga bao hilo kwenye dakika ya saba ya muda nyongeza. Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 72 na kuendeleza ‘gap’ la pointi tano kati yake ya vinara Yanga SC wenye pointi 77 wakati Azam FC wakiwa nafasi ya tatu na pointi 66. Kwa upande wao JKT Tanzania wamebaki na pointi zao 39 katika nafasi ya 13.