Azam FC, imelazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Alliance katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. Ilibidi Azam FC iweze kusubiri hadi dakika ya 79 kuweza kupata bao la uongozi, lililofungwa na Joseph Mahundi, aliyeingia dakika ya 76, kuchukua nafasi ya Ramadhan Singano, na alifunga bao hilo kiustadi akiunganisha krosi ya Chirwa. Dakika ya 90 Alliance ilisawazisha kupitia kwa Dickson Ambundo, akimalizia mpira uliogonga mwamba kufuatia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Israel Patrick. Azam walionekana kulalamikia bao hilo wakidai kuwa beki wao Agrey Moris alisukumwa kabla ya kufungwa lakini, mwamuzi Abubakar Mturo (Mtwara) na Msaidizi namba moja, Mohamed Mkono (Tanga), waliamuru kuwa bao halali.