WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwankyembe, leo alifanya ziara ya kutembelea Makao Makuu ya Azam FC ‘Azam Complex’ na kukiri kuwa timu hiyo ni kiwanda cha soka nchini. Ziara hiyo ya Mwakyembe ilikuwa ni maalumu kwa ajili ya kuangalia Azam FC ilipofikia kwenye uboreshaji wa uwanja huo ikiwa ni maandalizi ya kuelekea fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U-17) zitakazofanyika nchini mwakani. Uwanja wa Azam Complex ni miongoni mwa viwanja vitatu nchini vilivyoteuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kushirikiana na la hapa nchini (TFF), vingine viwili vikiwa ni Uwanja wa Taifa na ule wa Uhuru. Kigogo huyo aliambatana na Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Taifa (BMT), Alex Nkeyenge na Mkurugenzi wa Mashindano TFF, Salum Madadi, ambao walikaribishwa na wenyeji wao akiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Wakurugenzi, Nassor Idrissa ‘Father’, Makamu Mwenyekiti Omary Kuwe, Meneja wa timu, Philllip Alando. Akitoa neno kwenye ziara hiyo, Waziri Mwakyembe, aliupongeza uongozi wa Azam FC kwa kazi kubwa waliyofanya kwenye kuboresha uwanja huo kwa ajili ya fainali hizo ambazo zitafanyika kwa mara ya kwanza nchini. “Kwa kweli ni mara yangu ya kwanza kutembelea Azam Complex na nimejiridhisha mwenyewe kwamba hiki ni kiwanda cha soka, kiwanda cha michezo kuna kila kitu hapa na tukifikia hatua ambayo pengine timu zetu zenye sura ya Kitaifa hata zikawa tatu, nne, tano zikawa na mfumo ulioko hapa Azam Complex tayari sisi Tanzania tumeshakuwa nchi ya soka. “Na nadhani tutaanza kuuza wachezaji wengi sana duniani ambao pia watachangia sana katika pato la Taifa maana wenzetu wengi kama nchi ya Brazil inaendeshwa na pesa kama hiyo, Azam hongereni sana mmefanya kazi kubwa sana,” alisema.