Baada ya Yanga kuchapwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar,nahodha wa timu hiyiop Ibrahim Ajib amewatupia lawama waamuzi kuwa wamekuwa hawaitendei haki timu yao katika mechi nyingi za Ligi Kuu Bara. Bao la Riphat Khamis dakika ya 52 lilitosha kuipa ushindi Mtibwa Sugar na kuendeleza rekodi yao bora inapocheza nyumbani kwani katika michezo mitano mfululizo iliyopita iliyocheza Morogoro imeshinda yote. Kukataliwa kwa bao lililofungwa na Amissi Tambwe dakika ya 89 ndiko kulisababisha Ajib kutoa ya moyoni ukuhusu waamuzi kuwa wamekuwa hawatendi haki licha ya wachezaji kupambana sana uwanjani kutafuta matokeo. Mwamuzi Hans Mabena wa Tanga alikataa bao hilo baada ya kumuangalia mwamuzi wa pembeni ambaye alinyoosha kibendera kuashiriki mfungaji alikuwa ameotea. "Waamuzi hawachezeshi kwa haki kwani huwa hawako upande wetu mechi nyingi. Kwani tunajitahidi kwa uwezo wetu lakini inaumiza unapambana sana lakini anatokea mwingine anakurudisha nyuma"alisema. Ajib amesema wataendela kupambana katika michezo iliyobaki kwani licha ya wapinzani wao Simba ambao wanawafuukuza wana mechi nyingi hivyo lolote. Kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, Meddie Kagere amefunga mabao mawili na kuikoa timu yake isipate kipigo kutoka kwa Coastal Union. Simba ilijikuta ikishangazwa dakika ya kwanza tu baada ya Raizin Hafidhi kuifungia Coastal Union bao kutokana na beki Erasto Nyoni kujichanganya na kipa wake Aishi Manula katika kuokoa mpira huo. Kagere aliisawazishia Simba bao kwa penalti dakika ya 48, penalti iliyotokana na Emmanuel Okwi kuangushwa na kipa wa Coastal Union Sudi Mohammed. Dakika ya 68 Kagere aliipata Simba bao la pili kwa shuti kali akimalizia pasi ya Clatous Chama hivyo kufikisha mabao 16 kwenye ligi na kumfikia kinara Salum Aiyee wa Mwadui FC huku akimzidi bao moja Heritier Makambo wa Yanga mwenye mabao 15.