KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanya kweli baada ya kuidungua Mwadui bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliomalizika Uwanja wa Azam Complex usiku huu. Ushindi huo unaifanya Azam FC kusogea hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikifikisha jumla ya pointi 41 na kuishusha Yanga yenye mechi mbili mkononi hadi nafasi ya nne ikibakiwa na pointi zao 40 huku Simba ikiwa kileleni kwa pointi 46. Bao pekee la Azam FC limewekwa kimiani na mshambuliaji Yahya Zayd, dakika ya tano akitumia uzembe wa kipa wa Mwadui, Anold Massawe, aliyepiga mpira vibaya na kumpasia mguuni mfungaji wakati akiwa kwenye harakati za kuupiga mbele mpira aliorudishiwa na beki wake, Idd Mfaume.