Timu ya taifa ya Tanzania Bara Kilimanjaro Stars imepoteza mchezo wa kwanza wa Kombe la Cecafa Senior Challenge baada ya kukubali kufungwa bao 1-0 na Kenya kwenye mchezo uliochezwa katika uwanja wa KCCA nchini Uganda. Katika mchezo huo Kenya walifanikiwa kupata bao la mapema ambalo lilifungwa dakika ya 4 na Abdallah Hassan na kudumu hadi mchezo unamalizika. Kilimanjaro Stars walipambana kuhakikisha wanasawazisha bao hilo kwa kufanya mabadiliko mbalimbali ya kiufundi lakini jitihada zao ziligonga mwamba kutokana na umakini wa timu ya Kenya ambao walicheza kwa tahadhari kubwa kulinda bao lao. Kwa matokeo hayo Kilimanjaro Stars inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa kundi B ikifuatiwa na Sudan na Zanzibar Heroes huku Kenya wakiongoza kundi hilo.