Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba wamefuta uteja mbele ya Kagera Sugar baada ya kuvuna alama tatu uwanjani Kaitaba kufuatia ushindi wa mabao 3-0 walioupata jioni ya leo. Magoli ya Simba yamefungwa na Medie Kagere aliyefunga mawili dakika ya 4 na 79 kwa penati huku bao lingine likifungwa na beki Mohamed Hussein Zimbwe Jr. dakika 36. Medie Kagere anazidi kujikita kileleni mwa msimamo wa wafungaji akiongeza kibindoni mabao mawili kwenye mchezo huo na kufikisha mabao matano mpaka sasa. Mchezo kati ya Kagera Sugar na Simba ni miongoni mwa mechi zenye msisimko mkubwa kutokana na rekodi mbaya ya Simba msimu uliopita akikubali kipigo cha nyumbani na ugenini kutoka kwa Wanankurukumbi. Mbali na kupata ushindi huo pia wekundu wa msimbazi rasmi wameishusha Kagera Sugar kutoka katika uongozi wa msimamo wa ligi kutokana na utofauti wa magoli ya kufunga na kufungwa.